Tuesday, June 15, 2010

Kwanini Waafrika Hatujiamini?

Habari, ndg, jamaa na marafiki, samahani naomba leo nigusie kidogo juu ya tatizo la waafrika kutokujiamini mathalani Tanzania nikiingolea kama mwakilishi mkuu ktk hili.

Kutokujiamini ni hali yakujiona huwezi au hufai ktk kufanya jambo fulani au kufikiri kuwa fulani ni bora zaidi yako ktk kutimiza kitu au jambo fulani, na kutokujiamini huku kwaweza kuwa ktk masomo, ofisini au ktk biashara na shughuli zingine za kijamii. Mara nyingi kunahusiana na mwonekano wa mtu ktk watu au popote penye mkusanyiko wa watu, kwa mfano mwanafunzi waweza kuta anfahamu juu ya jibu la swali lilioulizwa darasani lakini kutokujiamini kwake kunamfanya ashindwe kujibu, au ofisini waweza kuta mchango fulani wa mawazo unahitajika na mtu akawa na mawazo mazuri lakini akashindwa kuyatoa kwa sababu tu ajiamini au ni kwa vile anahisi mawazo yake hayatapokelewa kama vile anavyotarajia.

Hili ni tatizo ambalo linawakwamisha watu ktk mambo mengi sana hususani yenye kuleta mafanikio au matunda chanya ktk jamii aliyomo, limekuwa tatizo sana ktk nchi zetu za kiafrika ukilinganisha na wenzetu wa mataifa yaliyoendelea, sasa jaribu kufikiria chanzo au kiini cha tatizo hili ni nini?

Tatizo hili kwa waafrika linamizizi toka ktk ngazi ya familia na wazazi ndio wa kwanza kulaumiwa ktk hili, nitatoa maelezo ya kina juu ya kwa nini nasema wazazi wamekuwa ndio rutuba mbaya ktk kukuza watoto ambao mbeleni wanashindwa kuweka imani kwao wenyewe.

Wazazi wetu wamekuwa ndio msingi wakutokujiamini kwetu, kwa mfano mara nyingi wamekuwa wakitupatia kauli zakutukatisha tamaa na kutufanya tujione kama hatuwezi lakini pia na wao wamerithi hili toka kwa wazazi wao, kwa mfano waweza kuta mtoto ana kipaji sana ktk soka lakini malezi na kauli za mzazi ndizo zinakuwa kauli mbiu ktk kuua kipaji cha mtoto, muda mwingine mtoto anachelwa kutoka mazoezini na wenzie, akifika nyumbani akimkuta baba ni kasheshe, atachapwa nakuambiwa kauli kama, "mpira utacheza wewe?" "we unafikiri kucheza kwako kote utaweza kuwa kama Christiano Ronaldo?"hizi ni kauli mbaya ambazo zinamfanya mtoto ajione kuwa hawezi kufanya chochote hata akijitahidi vipi hatoweza mfikia Christiano Ronaldo. Hatimae kipaji cha mtoto kinapotea, hii ni kinyume kabisa na nchi zilizoendelea kwani mtoto akionyesha uweza au hamasa ktk kitu fulani au kipaji fulani wazazi ndio wanakuwa mstari wa mbele ktk kuhakikisha wanatoa support yao ya mwisho ktk kukuza hicho kipaji, mfano rahisi ni wa kina Venus na Serena Williams ambao ni wacheza tenisi waliofanikiwa na maarufu duniani, wakati wanaonyesha nia na kipaji chakucheza tenisi familia yao ilikuwa maskini sana, lakini ili halikumzuia Baba yao kutoka na kwenda kuokota mipira pamoja nakujibana ili awanunulie vifaa vyakufanyia mazoezi mabinti zake, nyakati za awali iliwalazimu akina Venus kutumia mipira iliyotupwa baada yakutumika toka kwenye timu ya tenisi iliyokuwa mtaani kwao, lakini umaskini wa baba yao haukumzuia kumfanya awatafutie kocha mabinti zake ili awafundishe tenisi, jaribu kuona leo Venus na Serena wapo wapi ktk tenisi, je baba yao angedharau kipaji cha mabinti zake leo wewe ungemjua?ila mabinti hawa wamekuwa chachu ya maisha mazuri ya baba yao hivi sasa niandikapo mada hii.

Lakini hebu tujaribu kufikiria kwamba twawezaje kujenga hali hii yakujiamini? Jibu ni rahisi sana kwanza kabisa anza kumjengea mtoto au tujaribu kuwajengea watoto wetu mtazamo chanya ktk kuwaonyesha kuwa kila kitu kinawezekana na tuendelee kuwafanya waone hivyo ktk maisha yao yote, tuwafanye wajiweke ktk hali yakujifunza popote pale baya linapotokea aidha kwa kulifanya wao wenyewe au kumuona mwingine akiwa amelifanya, pia tuwaweke ktk nafasi yakuwafanya wasishindwe kujaribu ijapokuwa yawezekana walishindwa hapo mwanzo, misingi hii ni muhimu sana katika kumjenga mtoto nakumfanya ealewe kuwa kutojaribu ndio kushindwa na sio kushindwa baada yakujaribu.

Pia kitu muhimu ktk kumjenga mtoto ktk kujiamini ni kumshirikisha ktk shughuli muhimu, utafiti unaonyesha kuwa wale watoto wote ambao wameshiriki mara nyingi ktk aidha maharusi au send off kama wasimamizi ktk kuwaongoza maharusi au hata kuwa ma Mc ktk vipaimara au kumunio za wenzao wanajiamini sana tofauti kabisa na wale wasiowahi kujishughulisha ktk mambo hayo. Kumfanya mtoto aweze kuwaface watu wengi ktk jambo fulani iwe sherehe au nini kunamfanya mtoto huyo aanze kuzoea sura za watu na hivyo kumuondolea hofu hata pale atakapokua mtu mzima, wenzetu, jaribu kumuangalia Barack Obama, mabinti zake amekuwa nao bega kwa bega ktk kampeni zake za urais hadi siku anayoapishwa kama rais, je nikusema Obama anawapenda sana mabinti zake?, hapana, Obama kuna kitu anawajengea mabinti zake, ambacho marais wa nchi zetu hawakifanyi more often,pia kama umekuwa ukiangalia Tuzo mbalimbali za muziki USA mfano BET, utaona Lil Wayne mara nyingi ameongozana na binti yake wakati anaenda kupokea tuzo, na hii sio kwa Lil Wayne tu bali kwa wasanii wengine wengi pamoja na watu wengine maarufu.

Mfanye mtoto akupende sana na kukuheshimu na sio kumfanya mtoto akuogope sana na kukupenda kidogo huku akikupa nafasi ndogo yakukuheshimu, hili ni tatizo, kwani wazazi wengi Tanzania wanaogopwa na watoto wao, mfano unakuta baba akiingia sebuleni watoto wanatoka nakuingia vyumbani, je utaweza kweli kukaa na wanao kujua mahitaji au dukuku au hata maendeleo yao ya shule? pengine watoto wanaweza kuwa na ushauri mzuri hata ktk mambo yako ya maendeleo lakini wanashindwa kuyawasilisha mawazo yao kwako kwani wanakuogopa. Pia inashauriwa kuomba ushauri hata kwa watoto wako japokuwa ni wadogo kwani huwezi jua wanafikiria nini ktk akili zao.

Fanya mazoea yakupata muda wa pekee na watoto wako, ktk hili utawafanya wakuzoee na kuona kama wanaweza leta matatizo na kero zao kwako kirahisi, pia mwaweza hata kujadili mambo muhimu yanayohusu affairs zao. Sio kila siku wewe kama mzazi unarudi usiku tena umelewa, fahamu kuwa utakuwa unajenga msingi mbaya sana kwa wanao. Onyesha kuwa unawajali na thamini mahitaji yao, kaa nao na ikiwezekana wape mtazamo wako juu yao na matarajio yako kwa kila mmoja(kama unao zaidi ya mmoja), kwa kufanya hivi utawafanya watoto wako waweke nia ktk kuyatimiza matarajio yako juu yao. Pia wafanye wajione kuwa wao ni kiungo muhimu sana ktk maisha yako.

Kitu kingine ktk kujenga mtazamo na hali yakujiamini kwa watoto wako, siku zote epuka kuongea kauli mbaya mbele yao, weka tamaa yakuwaambia kuwa mambo yatakuwa mazuri ijapokuwa wewe mwenyewe unafahamu kuwa ukitarajiacho kiko mbali ktk kufanikiwa, waonyeshe kuwa kila kitu kinawezekana chini ya jua, na pia kutokufahamu kitu kusikupe wewe hali yakuona kuwa kitu hicho hakiwezekani, kwani kigumu kwako ni rahisi kwa mwingine, na kirahisi kwako ni kigumu kwa mwingine pia.

Naomba niishie hapo kwa leo, kikubwa zingatia uyafanyayo na uyazingumzayo kwa watoto wako wewe kama mzazi, kwani waweza zalisha mbegu mbaya ktk matunda mazuri yaliyotokana na mgegu yako mwenyewe.



muelimishaji2009

No comments:

Post a Comment